Tarehe 25 Mei 2025, mara baada ya ibada kumalizika, Mwinjilisti Eliud Ikwataki alimkaribisha Mchungaji Henry Mwinuka kuendesha semina maalum kwa viongozi wa jumuiya 16 zilizopo ndani ya Kanisa. Semina ililenga kuwaimarisha viongozi kiimani, kimaadili, na kiuongozi.

Mchungaji Henry Mwinuka, ambaye ni Mratibu wa Idara ya Misioni, Uinjilisti na Diakonia (MUD) katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani – KKKT, aliongoza semina hiyo akitumia mafundisho ya Biblia na uzoefu wake katika utumishi.
Katika mafundisho yake, Mchungaji Mwinuka alisisitiza umuhimu wa kiongozi wa jumuiya kuwa kielelezo cha maisha ya Kikristo. Alisema:
“Kiongozi wa Jumuiya lazima awe mfano wa kuigwa (‘role model’) kwa wale anaowaongoza. Kwa njia hiyo, wana Jumuiya watapata fursa ya kujifunza kwa matendo na maisha yake ya kila siku.”
Mchungaji.Henry Mwinuka
Lengo kuu la semina lilikuwa ni kuwajengea uwezo viongozi hao katika namna bora ya kuongoza jumuiya zao kwa ufanisi, kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na kuendeleza huduma ya kiroho katika ngazi ya msingi ya Kanisa

Semina hii iliandaliwa kwa mafanikio na Kamati ya Misioni na Uinjilisti ya Kanisa, kama sehemu ya juhudi endelevu za kukuza uongozi wa kiroho na kuimarisha huduma ya jumuiya katika mwili wa Kristo.

Tunaendelea kumshukuru Mungu kwa mafanikio ya semina hii, na kuwaombea viongozi wote waliohudhuria ili waendelee kuwa mwanga na chumvi ndani ya Jumuiya na jamii zao.